Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
(kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba
kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo
ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana.
……………………………………………………….
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
Serikali imeombwa kuongeza kiasi
cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na
Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi
milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo
ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na
baadhi ya vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na
halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza
kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za
mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na
kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za
shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali
kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji
cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne
kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na
kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa
ambalo ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni
na Nyakibimbili na kwenda kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na
changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka
na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa
kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia
jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na
magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa kikundi cha
Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na
laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi
chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na
bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha
kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
No comments:
Post a Comment