Kanuni
za Katiba ni kanuni ambazo zimepitishwa baada ya kupatikana kwa sheria,
hivyo wanatakiwa kwanza ama kurejea katika Bunge la Jamhuri.
Dar es Salaam.
Wakati Bunge Maalumu la Katiba
linakusudia kufanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wajumbe wa
Bunge hilo ambao wamesusia kushiriki mchakato wa Katiba, wanasheria,
wasomi na wanaharakati wamepinga dhamira hiyo wakisema itasababisha
kuvunjwa kwa Katiba.
Wajumbe
wanaolengwa katika marekebisho hayo ni wale wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kutoka Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe
kutoka Kundi la 201 walioteuliwa na Rais.
Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akizungumza na gazeti hili
mwishoni mwa wiki alisema mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha
masuala ya nidhamu, yakiwamo fujo na utoro, mambo ambayo hivi sasa
hayawezi kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa Bunge hilo.
Sitta
alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake juzi na
kusomwa mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya
Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya kikao cha usuluhishi alichokuwa
amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo unaotishia kukwamisha mchakato
wa Katiba Mpya.
Taarifa hiyo ilisema kitendo cha Ukawa
kuendelea kususia Bunge, kinapuuza wito wa jamii kupitia makundi
mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini na juhudi za usuluhishi za kutaka
kuwezesha vikao vya Bunge hilo viendelee.
Ukawa walitoka
bungeni siku chache kabla ya kuahirishwa kwa awamu ya kwanza ya Bunge
Maalumu Aprili 16 mwaka huu, kwa madai kwamba CCM kinatumia wingi wa
wajumbe wake kutaka kufutwa kwa baadhi ya mapendekezo ya wananchi
yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Tayari Mwenyekiti Ukawa,
Freeman Mbowe na Mwenyekiti Mwenza, Profesa Ibrahim Lipumba wamesisitiza
kuwa hawatarejea bungeni hata kama Bunge litafanyia marekebisho kanuni
ili ziwabane Ukawa.
Profesa Maina
Mtaalamu wa
Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Peter Maina
alisema kama wanataka kufanyia mabadiliko kanuni, kinachotakiwa
kufanyika kwanza ni kubadili sheria ya mabadiliko ya Katiba ili kanuni
zilizokusudiwa kufanyiwa marekebisho zisiwe juu ya sheria.
“Kanuni
za Katiba ni kanuni ambazo zimepitishwa baada ya kupatikana kwa sheria,
hivyo wanatakiwa kwanza ama kurejea katika Bunge la Jamhuri kufanya
marekebisho ya sheria, kisha ndiyo wafanye hayo marekebisho wanayoyataka
ya kanuni,” alisema Profesa Maina.
Aliongeza:
“Kinachotakiwa hapa ni watu kuheshimu sheria kama tunataka mchakato huu
umalizike salama na tupate katiba bora na yenye kuweka mbele masilahi ya
taifa.”
Profesa Shumbusho
Profesa wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe, George Shumbusho alisema jinsi mchakato ulipofikia hakuna
haja ya kuupeleka haraka na kinachotakiwa ni kuusimamisha na kufanya
marekebisho kwa Katiba ya sasa.
“Sijui haraka hizi za nini.
Hakuna haja ya kufanya marekebisho ya kanuni, tuifanyie marekebisho
Katiba ya sasa hasa vipengele vya uwepo wa tume huru ya uchaguzi kwa
ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015 na baada ya hapo sasa ndipo mchakato huu
uendelee tena, lakini sasa umekwama,” alisema Profesa Shumbusho.
Aliongeza:
“Kama Ukawa wametoka tatizo siyo kubadili kanuni tunatakiwa kupata
majibu kwa nini wametoka na katiba bora haiji kwa kubadili kanuni.”
Profesa
Shumbusho alisisitiza kuwa mchakato ulipofikia hakuna haja ya kuupeleka
haraka na kinachotakiwa ni kuusimamisha na kufanya marekebisho kwa
Katiba ya sasa.
“Sijui haraka hizi za nini, hakuna haja ya
kufanya marekebisho ya kanuni, tuifanyie marekebisho Katiba ya sasa hasa
vipengele vya uwepo wa tume huru ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa
mwaka 2015 na baada ya hapo sasa ndipo mchakato huu uendelee tena,
lakini sasa umekwama,” alisema Profesa Shumbusho.
Aliongeza:
“Kama Ukawa wametoka tatizo siyo kubadili kanuni tunatakiwa kupata
majibu kwa nini wametoka na katiba bora haiji kwa kubadili kanuni.”
Maria Kashondo
Maria
Kashondo aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema
Bunge hilo linachokifanya sasa ni batili kwa sababu idadi ya wajumbe
waliobaki ndani ya Bunge hawakidhi akidi inavyotakiwa kisheria.
Alisema
kosa lilianza kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano kufanya marekebisho ya
sheria kuhusu ukomo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani
ingekuwapo wajumbe wake wangekuwa wakifafanua baadhi ya vipengele
vinavyoonekana kutokueleweka vizuri.
“Walirekebisha sheria
ili Tume isiwepo, ingekuwapo haya yanayotokea yasingekuwapo. Lakini
marekebisho yanayofanywa na Bunge hilo likiwa pungufu ni batili, hata
yale yaliyokwishafanyika nayo ni batili,” alisema Kashonda.
Polepole
Aliyekuwa
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko Humphrey Polepole alisema Sitta anatakiwa
kuwa kama baba katika familia kwamba mtoto anapokosea hutakiwi
kumwadhibu bila kujua tatizo.
Alisema kama Ukawa wamegoma
kufika meza ya majadiliano Sitta hakutakiwa kuwa na hasira alitakiwa
kujishusha na kutumia busara na hekima kuwaita tena na wakigoma sasa
wananchi wataona nani ni mkorofi.
“Kilichotokea ni kutibu
matokeo badala ya kuangalia mzizi, tatizo lililopo katika Bunge Maalumu
la Katiba linatakiwa kuangaliwa kwa mapana na si juu juu tu, kwani kama
Tume nayo ingekuwa hivyo Rasimu iliyopo mezani isingepatikana,” alisema
Polepole ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi za kiraia nchini.
Mandari
Mratibu
wa Muungano wa Jinsia na Katiba wa Chama cha Wanasheria Wanawake
Tanzania (Tawla), Vicky Mandari alisema huwezi kufanya marekebisho ya
kanuni bila kuanza na marekebisho ya sheria.
“Uroho wa
madaraka ndiyo unatufikisha hapa. Kuna matatizo lukuki ya wananchi hasa
miundombinu ya elimu, maji, afya hivyo wanatakiwa kujikita kujadili
mambo haya na si kukimbilia kufanya marekebisho ya kanuni.”
“Bunge
hilo linatakiwa kujua kwamba wao siyo wenye uamuzi wa mwisho, kwani
hata wakifanya vipi bado wananchi ndiyo watakuwa na kauli ya mwisho
kuhusu Katiba Mpya. Tunawaomba waweke mbele masilahi ya taifa kabla ya
vyama vyao,” alisema Mandari.
Ngurumwa
Mratibu wa
Mtandao wa Wapiganiaji wa Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa alisema
katiba inavyoandaliwa inatakiwa kuyashirikisha makundi mbalimbali na
ikitokea kundi moja likasusia mchakato huo, hautakiwi kuendelea
kisheria, kwani utakuwa unakiuka Katiba ya nchi.
“Unapofanya
marekebisho ya kanuni ni lazima zilingane na sheria. Huwezi kuwa na
kanuni zilizo juu ya sheria, kwani wakifanya hivyo watasababisha vurugu
kama zilizotokea kwa wenzetu kule Kenya,” alisema Ngurumwa.
Aliongeza:
“Hapa mchakato umekwama na hakuna haja ya kubadili kanuni. Umefika
wakati wa Rais Kikwete (Jakaya Kikwete) kama mwenyekiti wa chama chake
(CCM) kuchukua uamuzi wenye kujali masilahi ya watu wote kwa kuukwamua
mchakato huu, bila hivyo hakuna kitakachoendelea.”
Mkazi wa
Kimara Dar es Salaam, Aivan Alfred alisema Julai 31 mwaka huu anakusudia
kufungua kesi ya kupinga kuendelea na vikao vya Bunge Maalumu la Katiba
kujadili Rasimu ya Katiba.
Alisema pingamizi hilo linatokana na Bunge hilo kujadili mambo ambayo ni kinyume na maoni yaliyotolewa na wananchi.
“Nitakwenda kusimama mahakamani kwa niaba ya Watanzania zaidi ya milioni 44.5 kupinga mjadala huo usiendelee.
“Hatuwezi
kuacha wao wajadili mambo ambayo si maoni yetu. Hili suala la Serikali
mbili halipo kwenye rasimu hata ukisoma sura ya kwanza hadi ya mwisho
hakuna kitu kama hicho,” alisema Alfred.
Alisema taasisi na
viongozi wa dini wamesema, lakini bado mambo yanaendeshwa kijanja janja
tu, Ninasema sasa basi, kwa miaka 50 tumekuwa na Katiba waliyoitaka wao
yenye viraka na upungufu lukuki, hivi sasa tunataka Katiba tunayoitaka
sisi.”
Hamad Salim, Mhadhiri Chuo Kikuu Huria
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Hamad Salim alisema kinachotakiwa
kufanyika kwanza kabla hata ya kuunda hizo kanuni ni makubaliano baina
ya pande hizo mbili.
“Makubaliano ndiyo msingi wa kupata
katiba tunayoitaka, lakini wanavyokimbilia kwenye masuala ya kanuni
haifai. Ukiangalia wanaoenda kutunga kanuni ni wale wale ambao wamekuwa
wakilinda masilahi yao wenyewe,” alisema Salim na kuongeza:
“Lakini
hii hali ilianza kudhihirika tangu hapo awali mchakato huu ulipoanza.
Tuliona kabisa hawa watu hawapo pale kwa ajili ya kutetea na kulinda
masilahi ya wananchi bali masilahi yao wenyewe na hicho ndicho
kinachoendelea sasa”
Alisema mambo yamekuwa yakipelekwa mbio
mbio, hakuna ushirikishwaji wa wananchi ambao ni yakinifu wenye kuwapa
elimu na ufafanuzi wa kila hatua ya mchakato kiundani kama
inavyostahili.
Mhadhiri huyo alisema kama hata hizo kanuni
zikiwekwa haziwezi kuwa tiba ya kupata suluhu na hatimaye kupata Katiba
wanayoitaka Watanzania.
“Ni bora huu mchakato uvunjwe. Tusubiri uchaguzi ujao wa 2015 upite halafu mchakato uanze upya.”MWANANCHI
No comments:
Post a Comment