Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwembetogwa, Kevin Mlengule |
SHULE
ya Sekondari ya Mwembetogwa ya Mjini Iringa imepongezwa na wadau wake
baada ya hivikaribuni kuwafukuza kazi walimu wanne wa kiume waliobainika
kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike.
“Tunataka
shule nyingine ziige mfano wa shule hii, tumefarijika kusikia imechukua
uamuzi huo na kwa kufanya hivyo tunaamini shule hiyo itakuwa salama kwa
watoto wetu wa kike,” alisema mmoja wa wazazi wenye watoto wanaosoma
shuleni hapo, Joachim Mwaikambo.
Mwaikambo
alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na
mabadiliko makubwa katika shule hiyo ambayo wanafunzi wake “tuliozoea
kuwaona wakizurula mitaani wakati wa masomo.”
Naye
Jacob Basil aliupongeza uongozi wa shule hiyo akisema; “unadhibiti
nidhamu ya wanafunzi na watumishi wake jambo linalotupa faraja wazazi
wenye watoto shuleni hapo.”
Akitetea
uamuzi huo, Mkuu wa shule hiyo, Kevin Mlengule alisema pamoja na walimu
hao shule iliwafukuza wanafunzi wa kike wawili waliobainika kukubuhu
kwa ngono.
Alisema
walimu na wanafunzi hao, walibainika kujihusisha na vitendo
vinavyobomoa maadili ya watumishi na wanafunzi baada ya kura ya siri
kupigwa dhidi yao.
“Katika
kuboresha nidhamu kwa watumishi na wanafunzi wawapo shuleni jambo moja
lililokuwa linatusumbua na tukaamua kulitafutia dawa kali ni la
mahusiano ya mapenzi kati ya walimu na wanafunzi, na wanafunzi na watu
wa mitaani,” alisema.
Alisema
miaka mitatu iliyopita lilikuwa ni jambo la kawaida kwa wanafunzi wa
kike kujihusisha katika mapenzi na walimu wao pamoja na watu wengine
kutoka mitaani.
Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wanafunzi wenye tabia hiyo kufuatwa “na wanaoitwa mabwana zao” shuleni muda wowote na kutoroshwa.
Alisema
hali hiyo ilichangia kuporomosha taaluma shuleni hapo na kufanya
matokeo ya wanafunzi wanaomaliza shule hiyo kuwa mabaya kwa muda mrefu.
Mlengule
alisema matokeo hayo yaliwafanya baadhi ya wazazi kuwahamisha watoto
wao kutoka katika shule hiyo na kuwapeleka shule nyingine.
“Shule
ilikuwa na wastani wa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita
2,500 kila mwaka, matatizo hayo na mengine yaliyokuwepo yaliifanya
ibakiwe na wanafunzi wasiozidi 600.” Alisema.
Alisema
katika kukabiliana na utovu wa nidhamu; “hatuna mzaha hata kidogo,
mwalimu na mwanafunzi atakayebainika akijihusisha na ngono katika
mazingira yoyote yale wote kwa pamoja tunawafukuza.”
Aliwataka wazazi waliohamisha wazazi wao shuleni hapo kutoihofia tena hali hiyo kwani imedhibitiwa vya kutosha.
No comments:
Post a Comment