Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeridhia kuongeza mashahidi wawili muhimu wa upande wa mashtaka katika kesi ya kihistoria ya dawa za kulevya zenye thamani ya Sh225 milioni.
Akitoa uamuzi wake jana kuhusu ombi la upande wa mashtaka, Jaji Grace Mwakipesile alisema anashindwa kuelewa kwa nini upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ombi hilo la msingi la kisheria, wakati kesi hiyo ikihamishiwa Mahakama Kuu. “Kinachonishangaza ni upande wa mashtaka kwa makusudi na uzembe walishindwa kuwasilisha maombi hayo ya kuongeza mashahidi wawili, wakati kesi ilipokuwa ikihamishwa,” alisema kwa mshangao Jaji Mwakipesile.
Jaji Mwakipesile aliongeza kuwa: “Kutokana na ukweli kwamba vidhibiti viliorodheshwa na mashahidi wawili walitajwa wakati wa kusikiliza kesi, mahakama hii inachukuliwa ushahidi huo siyo wa kutisha. Na kwa kuwa ushahidi huo ni muhimu katika kesi hii, nakubali ombi la kuwaongeza mashahidi hao kutoa ushahidi,” alisema Jaji Mwakipesile wakati akitoa uamuzi wake. Kesi hiyo inawakabili watuhumiwa tisa akiwamo raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa.
Mama Leila kabla ya kukamatwa Juni 2011 eneo la Mbezi, Dar es Salaam, pia alikuwa akitafutwa na Serikali ya Marekani kwa makosa kama hayo. Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Ben Ngare na Anthony Karanja ambao ni raia wa Kenya na Watanzania watano Sara Munuo, Alma Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi na Rajabu Juma. Mashahidi walioongezwa ni Bertha Mamuya kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambaye ndiye aliyezifanyia uchunguzi dawa hizo na kisha kuzifunga, pamoja na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Neema kutoka Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya ambaye pia ndiye mtunza vielelezo hivyo. Awali wakili wa utetezi, Evod Mmanda alitumia Kifungu cha 289 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kupinga hoja ya upande wa mashtaka ya kutaka kuongeza mashahidi wawili.
“Mheshimiwa Jaji, Prosecution (upande wa mashtaka) waliomba jana ahirisho ili waweze ku- file (kuwasilisha) hicho walichokiomba (taarifa ya kumwongeza shahidi), ruhusa umeitoa leo kwenye uamuzi wako, hivyo walitakiwa wa-file notice yao hiyo baada ya uamuzi wako (wa leo),” alisema na kuongeza: “Hivyo hakuna notisi halali hapa mahakamani. Notisi halali ni ile watakayoiwasilisha baada ya uamuzi wako. Kwa hiyo sisi tunasema kuwa hadi sasa hakuna notisi halali ya kuita mashahidi wa ziada. “Kama Mahakama yako itaikubali hii wanayoita notisi, ingawa sisi tunasema siyo notisi halali, basi tunaomba Mahakama yako ione kuwa haikutolewa ‘in a reasonable time’ (wakati mwafaka).”
“Hawa wanatajwa kuwepo katika mchakato tangu mwanzo. Mamuya anakiri kupokea kifurushi (bahasha yenye vielelezo) Juni 16, 2011, hadi leo ni miaka miwili na miezi mitatu imepita. Hivyo walijua uwepo wa Mamuya mapema. Huu si wakati mwafaka,’’ alisema Wakili Mmanda. Hata hivyo, alisema hawana maelezo ya maandishi ya Mamuya wala ya ASP Neema huku akidai kuwa maelezo ya ASP Neema yanaonyesha kuwa yameandikwa Juni 11, mwaka huu wakati hatua ya maelezo ya kesi ilishakamilika. Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila alidai kuwa katika kesi zote za jinai si jukumu la upande wa mashtaka kuwapatia upande wa utetezi nyaraka mbalimbali wanazokusudia kuzitumia katika kesi, bali Mahakama. “Notisi wanayoitaja iko mahakamani tangu jana, hivyo utaratibu uliotumika wao kupata nyaraka nyingine ndio unaotumika kuwapatia notisi hii. Hivyo hoja ya upande wa mashtaka kuchelewa kuwa ‘serve’ (kuwapatia) haina msingi,” alisema Wakili Mwangamila.
Alisema taarifa hiyo iko mahakamani kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 289 (1) na (2) cha CPA na kuiomba mahakama ione kuwa imewasilishwa katika muda mwafaka.
No comments:
Post a Comment