NAIROBI, Kenya
Hali si shwari, unaweza kusema hivyo kutokana na mapambano yanayoendelea ndani ya Jengo la Westgate, nchini Kenya, kati ya majeshi ya Serikali nchini humo na magaidi wenye silaha tangu Septemba 21 mwaka huu . Jengo hilo lilivamiwa na wapiganaji wa Al Shabaab ambao wanadaiwa kufikia 10 hadi 15, kusababisha mauaji ya watu 62, wengine 175 kujeruhiwa na kuwateka baadhi ya watu ambao hadi sasa wanawashikilia ndani ya jengo hilo.
Jeshi la Polisi nchini, limesema watu 10 wanashikiliwa na walikamatwa wakati wakipanda ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).Pia jeshi hilo limewaonya Wakenya dhidi ya utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wanaochangisha fedha ili kusaidia waathirika ambapo utoaji damu bado unaendelea Uhuru Park, jijini Nairobi.
Taarifa iliyotolewa na Kituo cha Televisheni cha Citizen nchini humo, kilisema magaidi sita wameuawa katika mapambano hayo na wengine waliobaki ndani ya jengo hilo, wanaweza kujisalimisha baada ya kuwazidi nguvu.Kituo hicho kimeongeza kuwa, wanajeshi watatu wa Kenya kati ya 11 waliojeruhiwa katika mashambulizi yanayoendelea ndani ya jengo hilo, wamefariki dunia na kubaki wanane.Mkuu wa Majeshi nchini humo, Jenerali Julius Karangi, alisema katika mapambano hayo hakuna kurudi nyuma hadi magaidi hao wajisalimishe wenyewe.
Raia wa nchi nyingine wahusishwa
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje nchini Kenya, Bi. Amina Mohamed, amesema mwanamke mmoja raia wa Uingereza anadhaniwa kuhusika na tulio hilo.Bi. Mohamed alisema, mbali ya mwanamke huyo pia kuna raia wawili au watatu Wamarekani ambao inasemekana ni miongoni mwa magaidi hao wa mtandao wa Al Shabaab. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilisema raia sita wa Uingereza wamethibitishwa kufa katika shambulio hilo.Ofisi inayohusika na Mambo ya Nje nchini Uingereza, ilisema ndugu wa karibu wa raia hao ambao wamepoteza maisha katika shambulio hilo, tayari wamepewa taarifa.
Pia ofisi hiyo ilifafanua kuwa, haina taarifa zozote juu ya raia wao kuhusika na shambulio hilo, lakini bado wanaendelea kushirikiana na mamlaka za Kenya ili kuwasaidia katika uchunguzi kutokana na shambulio hilo la kinyama. Akizungumza na waandishi wa habari nchini Pakistan, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Theresa May, alisema "Nimepata taarifa kuwa mwanamke raia wa Uingereza amehusishwa na tukio hili."Tutathibitisha taarifa hizi kama uchunguzi utakamilika, si rahisi kukubali au kukanusha kwa sasa," alisema May.
Jeshi la Kenya
Hadi jana mchana, Jeshi la Kenya lilikuwa katika hatua za mwisho kukamilisha msako wa kulikomboa jengo hilo mikononi mwa magaidi.Shirika la Habari nchini Ufaransa (AFP), lilisema majeshi ya Kenya yalikuwa yakikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa magaidi wawili walioosalia ndani ya jengo hilo kila mmoja akiwa amejificha eneo lake. Milio ya risasi na milipuko ilisikika jana asubuhi katika jengo hilo, lakini Serikali ya Kenya, haijatoa idadi kamili ya mateka waliookolewa katika shambulio hilo.Kwa mujibu wa Kituo cha Televisheni cha K24 nchini Kenya, jana kilitangaza majina sita ambayo ni miongoni mwa magaidi wanaodaiwa kuhusika na shambulizi hilo.
Washukiwa hao ni Sayd Nuh (25), anayetoka Kismayu, Isamil Galed (23), Finland, Mustafa Noordiin (24) na Abdifatah Osman (24) wote raia wa Marekani, Kassim Musa (22), Garissa na Mohammed Badr (24), ambaye ni raia wa Syria.
Al Shabaab ni nani?
Jina Al-Shabab linamaanisha kijana kwa lugha ya Kiarabu. Kundi hilo liliibuka kama tawi la vijana la muungano wa mahakama za Kiislamu ambao baadaye ulivunjika mwaka 2006 baada ya kupigana na wanajeshi wa Ethiopia waliokuwa wameingia nchini Somalia kuyaunga mkono majeshi ya Serikali. Kundi hilo limeweka sheria kali za Kiislamu katika maeneo wanayoyadhibiti ikiwemo ya kupigwa mawe hadi kufa wanawake wanaodaiwa kufanya uasherati na kuwakata wezi mikono.Ingawa kundi hilo limepoteza udhibiti katika baadhi ya miji mikubwa nchini Somalia, liliondoka Mji Mkuu Mogadishu Agosti 2011 na Mji wa Kismayo Septemba mwaka 2012.
Kismayo ulikuwa mji muhimu wa kundi hilo na uliwawezesha kufikiwa na bidhaa pamoja na kuwatoza watu ushuru kwa shughuli zao.Kundi hilo lilianza kufanya mashambulizi ya kuvizia baada ya kushindwa na Majeshi ya Muungano wa Afrika wanaotumia nguvu dhidi yao ambapo Kenya ilianza harakati za kulimaliza kundi hilo mwaaka 2011 Kenyailiwatuhumu wapiganaji wa Al Shabaab kwa kuwateka nyara wanajeshi wake pamoja na watalii.
Nani kiongozi wa Al-Shabaab?
Ahmed Abdi Godane ndiye kiongozi wa kundi hilo ambaye anajulikana kama Mukhtar Abu Zubair, akitokea katika Jimbo la Somaliland. Kumekuwa na taarifa za mgawanyiko katika kundi hilo, ambazo hata hivyo, zinapingwa vikali na kundi lenyewe. Kiongozi wa kundi hilo Godane huwa haonekani hadharani, ambapo mtangulizi wake, Moalim Aden Hashi Ayro, aliuawa katika shambulizi lililofanywa na Marekani mwaka 2008.Al Shabaab walijiunga na al Qaeda, Februari mwaka 2012, ambapo kiongozi wa Al Shabaab (Godane), aliahidi kumuunga mkono kingozi wa al Qaeda, Ayman al-Zawahiri. Makundi hayo mawili yamekuwa yakifanya kazi kwa pamoja na baadhi ya raia wa kigeni wamekuwa wakiweaunga mkono na kuwasaidia katika harakati zao za mapigano
|
Thursday, September 26, 2013
UGAIDI KENYA : NGOMA NZITO -JESHI LASISITIZA HAKUNA KURUDI NYUMA HADI MWISHO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment