Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Singida Mjini, Mohammed Dewji amesema mangumbaru (watu wenye machachari, matata na fujo) wa siasa wanamchafua, kwa lengo la kuchukua kiti chake cha ubunge. Dewji, maarufu kwa jina la Mo, ametoa kauli hiyo wakati akifanua juu ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya watu waliodai ni wakazi wa Singida, waliodai eti kwamba hajafanya chochote cha maendeleo katika jimbo lake tangu achaguliwe kuwa mbunge. Tuhuma na malalamiko hayo yaliyotolewa na baadhi ya watu waliodai ni wananchi wa Singida kupitia mtandao wa Facebook, wakati wa kubadilishana mawazo na mbunge huyo. Pia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) aliwataka wana-Singida kuungana na Watanzania wengine kufanya maandamano kudai ahadi ya maisha bora kwa wote kama ilivyoahidiwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoko madarakani. Lema akiwa na wabunge wenzake, Chiku Abwao na Regia Mtema (Chadema - Viti Maalumu), alisema hayo wiki hii mjini Singida kwenye mkutano wa hadhara, huku akidai umefika wakati kwa wananchi wa Mkoa wa Singida ambao ni ngome ya CCM, kukiondoa chama hicho madarakani. Katika michango yao kwenye Facebook, wananchi hao walioruhusiwa kutoa maoni na dukuduku zao kwa Dewji, walidai kutoona maendeleo yoyote katika jimbo hilo kwa madai kwamba wananchi wa Singida wamekuwa wakiteseka na maisha kwa kukosa maji, ajira na masuala ya maendeleo. Katika ufafanuzi wake kuhusu malalamiko hayo, Dewji alisema tangu kuchaguliwa kwake amekuwa mstari wa mbele kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwenye maeneo ya kero za maji. Dewji alisema amefanikisha uchimbaji wa visima virefu zaidi ya 21 kwenye kata za Unyambwa, Mungu Maji, Unyamikumbi, Mwankoko, Mtamaa, Mandewa na Mtipa pamoja na baadhi ya kata za Mjini kama Kindai, Mitunduruni na Utemini. Dewji pia aliongeza kuwa bado anaendelea na jitihada za kukabiliana na tatizo hilo kwa kuibana Serikali itekeleze mradi mkubwa wa Benki ya Dunia wa kuchimba visima 10 jimboni na anaendelea kuibana Serikali ifanye haraka kumalizia mradi mkubwa mwingine wa maji unaofadhiliwa na Benki ya BADEA na OPEC. "Mradi huo ukikamilika ndio utakuwa ufumbuzi wa tatizo la maji Manispaa ya Singida... Mradi huu utabadilisha miundombinu yote ya maji safi ndani ya manispaa yetu. Unatarajia kukamilika mwaka 2013 na utagharimu takriban sh. bilioni 20," alisema Dewji. Kuhusu ajira, Dewji alieleza kuwa amekuwa mstari wa mbele kutoa Ajira kwa vijana kupitia kampuni yake ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) sambamba na kampuni nyingine mbalimbali. Alifafanua zaidi kuwa yuko mbioni kuwekeza katika jimbo lake kwa kufungua kiwanda kitakachotoa fursa zaidi kwa vijana na wakazi wa Singida kujipatia maendeleo na ajira, na kwamba kwa sasa anaendelea kuwasiliana na wataalamu mbalimbali wa uwekezaji ili kuona kama kuna fursa za kuwekeza katika manispaa ya hiyo. Alipongeza kupokelewa kwa mwito wa kuhamasisha michezo katika jimbo lake na kusisitiza kuwa ataendelea kunyanyua na kuibua vipaji kupitia mashindano yake yajulikanayo kama Mohammed Dewji Cup yakiwa na takriban miaka saba na yamekuwa na mafanikio makubwa kwa vijana wazaliwa wa Singida. "Kuhusiana na suala la ujenzi wa Uwanja wa Namfua, nilishaanza ukarabati katika eneo la jukwaa kuu, wananchi ni mashahidi... kama wanaufahamu uwanja ulivyokuwa mwanzo na wakati wa mashindano ya riadha kitaifa, nilikarabati eneo la kukimbilia wanariadha. "... Bado nitaendelea kukarabati kwa awamu mpaka tutakapoukamilisha. Ukumbuke ahadi hii haikuwa yangu peke yangu. Lakini nimeshanunua nyasi za bandia ambazo zimenigharimu sh. milioni 250... Natarajia kuziweka hizo nyasi mwaka 2012/2013," alisema Dewji.
No comments:
Post a Comment