“Mazunguzo siku zote ni ‘give and take’ yaani
kulegeza msimamo katika baadhi ya hoja badala ya kila upande kushupaa
kwa kile unachokiamini. Tukiwa na nia ya dhati ya kuzungumza,
tukashauriana, tukaridhiana na kukubaliana jinsi ya kutekeleza yale
tuliyoafikiana, basi Taifa litapata Katiba bora hivyo kuondoka katika
mkwamo wa sasa.
“Kwa sauti moja, tunapenda tena kumsihi Mheshimiwa Rais
kuahirisha mchakato huu ili kwanza kupisha maridhiano na pili kuokoa
fedha zinazotumika kwa ajili ya kusukuma mbele mchakato huu”.
Alisema kuna kila dalili kwamba hivi sasa Bunge
Maalumu linafanya kazi ilimradi lifike mwisho na ionekane kwamba kazi ya
kupata Katiba Mpya imefanyika akisema anaamini hawako katika njia
sahihi na wanawadhulumu Watanzania ambao wamewapa dhamana ya
kuwawakilisha.
“Kwa kuwa Katiba ni moyo wa nchi, tusifanye kazi
kwa kulipua ilimradi tuwapendeze wachache walioweka masilahi binafsi
mbele. Tukifanya hivyo tutakuwa tunaliweka Taifa rehani na baadaye
litaachwa liharibikie mikononi mwetu, sisi vijana.”
Alisema uchambuzi wa Rasimu unaoendelea ndani ya
kamati za Bunge hilo unakabiliwa na changamoto ya muda kwani zinatakiwa
kujadili sura na ibara nyingi katika muda mfupi kuliko walivyofanya
katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo. Alisema ikizingatiwa siku 16
walizopewa kwa ajili ya kujadili na kuchambua sura 15 zenye ibara 240,
ambazo ni wastani wa Ibara 15 kwa siku, ni dhahiri kazi haitafanyika
kwa weledi na kutoa Katiba bora... “Uchambuzi huu wa sasa hauwezi
kutuletea Katiba bora iliyokusudiwa.”
Ikulu: JK hana mamlaka kuvunja Bunge
Wakati Ladislaus akitoa wito kwa Rais kulivunja
Bunge hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu amesema
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haina kipengele kinachompa Rais uwezo wa
kufanya hivyo na kusisitiza kuwa mchakato wa Katiba umeanzishwa kisheria
na utamalizika kwa mujibu wa sheria hiyo.
Alisema ni ajabu kuona watu waliosema Rais
alifanya makosa kutoa maoni yake wakati akifungua Bunge hilo, kuibuka na
kumtaka Rais huyohuyo asitishe Bunge hilo.
“Bunge halitasitishwa na shughuli zake zitaendelea
kama kawaida. Hakuna sheria inayomtaka Rais asitishe Bunge, haipo
mahali popote,” alisema Rweyemamu.
Alipoulizwa iwapo Rais anaweza kutumia mamlaka
aliyo nayo kusitisha Bunge hilo, Rweyemamu alisisitiza kuwa sheria ndiyo
inayotakiwa kufuatwa. “Kila siku watu wanawazungumzia Ukawa, mbona
wajumbe wanaoendelea na vikao vya Bunge hilo hamuwatazami? Ukawa ni
kundi dogo zaidi ikilinganishwa na kundi lililopo bungeni,” alisema.
Wasira, Mnyika watofautiana
Mbali na Rweyemamu, wajumbe wawili wa Bunge la
Katiba, Stephen Wasira na John Mnyika jana walitofautiana kwa hoja
kuhusu mamlaka ya Rais kuvunja Bunge hilo.
Wakati Wasira akisema Rais hana mamlaka kisheria,
Mnyika alisema kuna njia mbili ambazo Rais akiwa mkuu wa nchi anaweza
kuzitumia kusaka maridhiano huku Bunge hilo likiwa haliendelei na vikao
vyake
Wasira ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na
Uratibu, alisema katika kipindi cha ‘Tuongee Asubuhi cha Star TV kuwa,
sheria haimpi uwezo Rais kulivunja Bunge na wanaodhani kwa kuwahamasisha
wananchi waandamane kulivunja wanajidanganya.
Mnyika alisema kuna dhana mbili ambazo
zinapotoshwa lakini zikitumika vizuri zinaweza kuuvusha mchakato huu
kutoka katika matumaini hasi kwenda chanya.
“Rais kama mkuu wa nchi anaweza kabisa kutumia
madaraka yake kwa masilahi ya wengi ama kulivunja au kuliahirisha Bunge
kupisha maridhiano,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo
(Chadema).
Alisema mbali na njia hiyo, inaweza kutumika njia
aliyoitumia Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuliahirisha Bunge
kuanzia Agosti 5 hadi Septemba 2 mwaka huu kupitisha kanuni, pia anaweza
kufanya hivyo kwa kipindi kirefu ili kupisha majadiliano.
“Rais Kikwete na Sitta kwa mamlaka waliyonayo
wangeweza kuliahirisha kama walivyoliahirisha sasa, hadi Novemba au
zaidi ya hapo ili kuwezesha majadiliano kuendelea.
“Lakini pia, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba siyo
kwamba haimpi Rais mamlaka hayo, yeye ndiye aliyeisaini na yeye kama
Mwenyekiti wa CCM aliliongoza Baraza la Mawaziri kuipitisha na kuileta
bungeni sasa kwa nini asiwe na uwezo wa kulivunja au kuliahirisha?”
alihoji.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania,
Deus Kibamba alipendekeza Rais Kikwete kwa kushauriana na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wapunguze idadi ya siku ambazo Bunge
litafanya vikao vyake kutoka 84 hadi chini ya hapo (hakufafanua) ili
kubana matumizi.
Kanisa: Mchakato wa Katiba uendelee
Kanisa la Baptisti Tanzania nalo limepingana na
makundi ya wananchi yanayotaka mchakato wa Katiba usitishwe likisema
uendelee kwa kuwa tayari mamilioni ya fedha za Watanzania yametumika.
Msimamo huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa
Makanisa ya Kibaptisti Tanzania, Mchungaji Ernest Sumisumi katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Kanisa hilo
Kinondoni B, Dar es Salaam.
Alisema kanisa halitaki mchakato wa Katiba
usitishwe kwa sababu ya mgawanyiko wa wajumbe na kuusitisha ni kuwatia
hasara wananchi.
Alisema kanisa linatoa wito kwa viongozi wa pande
zote mbili kuendelea kufanya mazungumzo ili kuwe na maridhiano ya pamoja
ambayo yatawafanya wajumbe wa Ukawa kurudi bungeni.
Chanzo;Mwananchi