Zitto na Demokrasia
Azimio la Mtwara Uwajibikaji katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi yetu.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi za bara la Afrika imejaaliwa kuwa
na Rasilimali mbali mbali za asili. Miongoni mwa rasilimali hizo ni
pamoja na Madini na Gesi Asilia. Usimamizi wa uvunaji wa rasilimali hizi
umegubikwa na manung’uniko makubwa ya wananchi hususan kutokana na
usiri mkubwa uliopo kwenye mikataba ya uvunaji wa Maliasili hizi za
Taifa. Mikataba yote 6 ya uvunaji wa Dhahabu bado ni Siri kubwa na vile
vile mikataba yote 26 ya utafutaji na uvunaji wa Gesi Asilia na Mafuta.
Mikataba miwili imevuja mpaka sasa na yote imeonyesha tofauti kubwa sana
na mikataba ya mfano ambayo Serikali imeweka wazi. Mikataba ya mfano
hutumika kujadiliana na makampuni ya uwekezaji katika utafutaji na
uchimbaji wa Gesi na Mafuta hapa nchini. Mageuzi katika sekta ndogo ya
gesi na mafuta yamekuwa hayashirikishi wananchi na hufanywa kwa usiri
mkubwa na hivyo kusababisha wananchi kutokuwa na taarifa kabisa na
kinachoendelea katika utajiri wao wa asili.
Mwaka 2007 nilitangaza Azimio la Songea lililokuwa na malengo makuu manne
1) kutokuwa na mikataba mipya ya madini mpaka mikataba iliyokuwepo
ipitiwe. Mikataba yote ya madini ilipitiwa na Kamati ya Bomani na tangu
mwaka 2007 hapajawa na mkataba Mpya wa madini ulioingiwa na Serikali.
2) kufanya mabadiliko ya sheria zote za kodi ambazo ni kikwazo katika
kukusanya kodi katika sekta ya madini. Sheria husika zimefanyiwa
marekebisho ikiwemo kupandisha mrahaba, kufuta nafuu ya kodi ya ongezeko
la thamani kwa kampuni za madini na kuirejesha kodi ya ongezeko la
mtaji.
3) Serikali kumiliki sehemu ya hisa katika migodi ya madini. Kwa
mujibu wa sera Mpya ya madini ya mwaka 2009 na sheria Mpya ya madini ya
mwaka 2010 Serikali itakuwa na hisa katika kila mgodi Mpya unaoanza
nchini.
4) Halmashauri za Wilaya zenye migodi kupata mgawo wa theluthi ya
mrahaba unaokusanywa katika madini yanayovunwa nchini. Pamoja na kwamba
hivi sasa Halmashauri zinakusanya kodi ya ‘ cess’ lakini bado Serikali
Kuu inabeba fedha yote ya mrahaba.
Malengo haya yaliongoza mjadala wa masuala ya madini mwaka 2007 mpaka
2010 sheria Mpya ya madini ilipotungwa. Utekelezaji wa Azimio la Songea
ni wa zaidi ya 75% lakini bado kilio cha wananchi kipo pale pale. Hii
inatokana na usiri mkubwa wa mikataba na hususan mikataba ya gesi na
miundombinu yake. Usiri huu unasababisha ukosefu mkubwa wa uwajibikaji
kwa upande wa watendaji wa Serikali. Usiri hupelekea rushwa na ufisadi.
Moja ya sababu kubwa zinazotolewa na watetezi wa usiri wa mikataba ni
kwamba mikataba ile ina Siri za kibiashara na hivyo washindani wa
kibiashara wataiba Siri za wenzao. Hoja hii ni nyepesi sana kwani
makampuni yote makubwa yanayowekeza nchini yamesajiliwa katika masoko ya
hisa kwenye nchi za magharibi na katika masoko hayo mikataba yao
hulazimika kuwekwa wazi. Hivyo usiri huo ni kwa wananchi tu na sio kwa
hao washindani. Makampuni mengi yaliyopo nchini yanamilikiwa na watu
wale wale kupitia masoko ya hisa. Vile vile majirani zetu kama Msumbiji
wameweka mikataba yao yote wazi.
Ni dhahiri kwamba moja ya sababu kubwa ya kushamiri kwa rushwa nchini
kwetu ni ukosefu wa mfumo thabiti wa uwajibikaji. Ndio maana katika
mkutano wa kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka 2015 uliofanyika
mjini Mtwara tarehe 31 Desemba 2014, niliwaomba wananchi wa Mtwara
kuufanya mwaka 2015 kuwa ni mwaka wa kuwajibishana. Hivyo Azimio la
Mtwara ni wito wa kutaka Uwazi na Uwajibikaji katika utafutaji na
uvunaji wa mali asili za nchi yetu. Azimio la Mtwara lina malengo
yafuatayo
1 kutaka mikataba yote inayohusu uvunaji wa rasilimali za nchi iwekwe
wazi kwa wananchi na Bunge liipitie kuidhia kabla ya kuingiwa kwa
mikataba hiyo
2 kutaka haki ya wananchi kuruhusu utafutaji wa madini au gesi na
mafuta katika maeneo yao ( right of free prior informed consent )
3 kutaka sehemu ya mrahaba unaotokana na uvunaji wa Maliasili ya nchi kugawanywa kwa maeneo yanayovunwa rasimali hizo
4 kutaka mfumo wa mapato na matumizi ya mapato yasiyo ya kikodi (
rents ) yanayotokana na uvunaji wa Maliasili za nchi kuwa wazi kwa
wananchi na kushirikisha wananchi katika kupanga matumizi husika kwa
faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo
Azimio hili ni wito tu utakaotusaidia kuiwajibisha Serikali katika masuala ya utajiri wa Taifa.
Zitto Kabwe, Mb
Mtwara 31-12-2014
No comments:
Post a Comment