N.I.H.F -KIKOA

N.I.H.F -KIKOA
N.I.H.F -KIKOA

FOREPLAN CLINIC

FOREPLAN CLINIC
FOREPLAN CLINIC

Wednesday, May 23, 2012

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Yapitia Ripoti ya Sheria Zinazosimamia Mfumo wa Haki za Madai

  

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Buxton Chipeta akitoa ufafanuzi wakati wa mkutano wa kupitia Ripoti za Sheria zinazosimamia Mfumo wa Haki za Madai jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa Mkutano wakimsikiliza Jaji Mstaafu Chipeta

Na Munir Shemweta
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kupitia ripoti za Mapitio ya Sheria zinazisimamia mfumo wa haki za Madai kwa lengo la kufanya maboresho ya sheria hizo.
Katika Mapitio hayo Tume kwa kushirikiana na wadau ambao ni wakufunzi wa vyuo, Taasisi zinazotoa misaada ya kisheria, Wanasheria, Mawakili na Mahakimu kwa pamoja itapitia ripoti zilizofanyiwa kazi na Wataalamu washauri.
Katika mchakato huo Tume imegawa makundi manne yatakayopitia ripoti hiyo katika mikoa ya Mwanza ambapo kundi hilo linaongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Profesa Ibrahim Juma, Arusha Kamishna wa Tume Ester Manyesha, Mbeya Kamishna wa Tume Profesa Sufian Bukurura, Dodoma Kamishana Ernest Mwipopo na Dar es Salaam linaloongozwa na Jaji Mstaafu Praxon Chipeta..

NMB NA SERENGETI ZAICHANGIA TWIGA STARS MILIONI THELATHINI

Katika kuendeleza soka Tanzania, leo hii Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya Bia ya Serengeti imesaidia maandalizi  ya Twiga Stars kwa kutoa  jumla ya shilingi Milioni Thelathini. Pia NMB na Serengeti wamekabidhi vifaa  vyenye  thamani ya Milioni Tano kwa timu hiyo ya Twiga Stars.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa idara ya Masoko na Mawasiliano wa NMB Bw. Imani Kajula alisema; NMB imekua  mbele  katika  kuchangia soka Tanzania, leo hii NMB ikishirikiana na Serengeti tunachangia maandalizi ya Twiga Stars”.
NMB inatambua kuwa Twiga Stars ikiwezeshwa inaweza ikafanya vizuri zaidi. Ili kutimiza lengo hili, NMB Ikiwa ndiyo  benki yenye mtandao mpana wa matawi mengi Tanzania nzima pia imeanzisha akaunti maalum kwa ajili ya kuchangia Twiga Stars. Yeyote atakayeguswa kuchangia Twiga Stars anaweza kuchangia kupitia akaunti namba 22310001185 yenye jina CHANGIA TWIGA STARS ACCOUNT
 Naibu Mkurugenzi wa michezo, Bi. Juliana Yasoda (kulia) akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa  Mkurugenzi wa Masoko wa Serengeti, Bw. Ephraim Mafuru (kati) na Mkuu wa Idara  ya  Masoko na Masiliano wa NMB, Bw. Imani Kajula (Kushoto). Wanaoshuhudia  tukio hilo ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bw. Sunday Kayuni (pili kushoto) na kocha msaidizi wa Twiga Stars Bi. Nasra Mohamed.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba atembelea Makao Makuu ya Vodacom Tanzania

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba akizungumza na watendaji wakuu wa kampuni ya Vodacom (hawapo pichani) wakati alipotembelea makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es salaam katika ziara maalum ya kujifunza shughuli za mawasiliano nchini. Kulia na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza.

MARC, MARAS, MADC WAONYWA KUWA WAADILIFU


WAKUU wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wameonywa juu ya haja ya wao kuwa waadilifu katika nyadhifa walizonazo kwani uongozi wa umma hauwezi kutenganishwa na maadili ya uongozi.
 
Wito huo umetolewa leo (Jumatano, Mei 23, 2012) katika mada tatu zilizowasilishwa leo kuhusu maadili kwa viongozi wa umma kwenye mafunzo maalum ya siku 10 kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na Wakuu wa Wilaya. Mafunzo hayo ambayo leo yamefikia siku ya tatu yanafanyika kwenye ukumbi wa St. Gaspar mjini Dodoma.
 
Akitoa mada kwa viongozi hao, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji (Mst.) Salome Kaganda alisema uadilifu ni zaidi ya kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na akawataka viongozi hao kuonyesha njia kwa matendo na mwenendo mwema ili waweze kuwasimamia watendaji walio chini yao.
 
Naye Askofu Mkuu Mstaafu, Mhashamu Donald Mtetemelwa aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na matumizi mabaya ya mamlaka walinayo kwani wasipofanya hivyo wanaweza kujikuta wakiwaumiza wengi. “Lengo la kiongozi ni kubeba maumivu ya watu na siyo kupeleka maumivu kwa wananchi,” alisema.
 
Alisema Tanzania kwa sasa inakabiliwa na tatizo la kukosa viongozi wengi walio waadilifu kwa sababu wengi wao wamemuacha Mungu kwa kisingizio cha kuwa na majukumu mengi. “Watu wakipewa madaraka wanajitenga na Mungu, lakini lazima wakumbuke kuwa uadilifu wao utategemea ni kwa kiasi gani wanamcha Mungu,” aliongeza.

WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO WAIOMBA SERIKALI KUWATENGEA SOKO MAALUM ILI KUEPUKA ADHA INAYOWAKUMBA

 
WAJASIRIAMALI wadogo wameiomba serikali kuwatengea soko maalumu ili waondokane na adha mbalimbali wanazokumbana nazo, ikiwemo ya kutojulikana kwa bidhaa zao.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kwenye Maadhimisho ya siku ya Afrika walisema licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali hususan katika kutangaza bidhaa zao, lakini bado jamii imeshindwa kuziamini bidhaa zao kutokana na kutokuwa na nembo ya ubora, ‘TBS’.
 
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Juliana Massawe alisema kuwa mbali na wajasiriamali hao kuendesha biashara zao katika mazingira magumu, lakini wanakabiliwa na tatizo la kutokuwa na nembo maalumu inayotambulisha bidhaa zao kama zina ubora unaotambulika, jambo ambalo huwalazimu kutoa elimu kwa wateja kabla ya kuwauzia.
 
Aidha, alilitaja baadhi ya changamotozinazowakabili ni jinsi ya upatikanaji wa vifungashio ambapo kwa sasa vinapyikana kwa gharama kubwa.
 
“Unajua hivi sasa tuko katika wakati mgumu wa upataji wa vifungashio, ukweli kwamba wachina wanapovikisha hapa bei yake inakuwa hali inayotulazimisha kupandisha gharama ya bidhaa zetu ili tupate faida”alisema Masawe.
 
Magesa Amani alitoa wito kwa watanzania kujenga ustaarabu wa kununua bidhaa zinazotengenezwa nchini kwani zina ubora ukilinganisha na baadhi ya zile zinazotoka nje.
 
Naye Mratibu wa maadhimisho hayo, Deus Stevin alisema kuwa maadhimisho hayo ufanyika kila mwaka 26 Mei kwa lengo la kumbukumbu ya uhuru wa Mwafika.
 
Vile vile Stevin alikiri kuwepo kwa tatizo la vifungishio pamoja na soko maalumu, ila akasema kwa sasa wameandaa mfumo wa kutoa elimu kwa wajasiriamali kabla hawajaangalia mtaji ili kumuandaa kwa ajili ya ubunifu wa bidhaa zenye ubora.
 
“Kabla hatujaangalia mtaji, tunaangalia ubora wa bidhaa yenyewe kwa lengo la kudhibiti, hata hivyo tunatoa na elimu ya mafunzo, soko la pamoja pamoja na usafi wa kufunga bidhaa” alifafanua Stevin.
Hata hivyo alifafanua kuwa tatizo la vifungishio si kwa wajasiriamali wa mjini tu, bali tatizo hilo linawakabili hata wale wa vijijini, hivyo kuna haja ya serikali kuangalia namna ya kutafuta wadau mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo sugu.
 
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Mei 26 katika viwanja vya mnazi mmoja na kufungwa na waziri wa Biashara,viwanda na masoko Abdallah Kigoda.

MKAZI WA JIJI APANDISHWA KIZIMBANI KWA UNYANG'ANYI

MKAZI wa jijini Dar es Salaam Humphery Mwankemwa amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa  la kutumia nguvu na kuiba mali yenye thamani ya sh.milioni 112.9 katika ubalozi wa Sudan nchini Tanzania.
Mwendesha Mashtaka wa serikali,Aidah Kisumo alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Tarsila Kisoka alidai kuwa mtuhumiwa  huyo alitenda kosa hilo Mei 6 eneo  la Ubalozi  wa Sudan barabara ya Ally Hassan Mwinyi  jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa Mwankemwa aliiba fedha taslimu sh. milioni 7.2 na dola za Kimarekani 71000, ambazo  fedha zote hizo zina thamani ya sh milioni 112.9.
Baada  ya kusomewa  mashitaka hayo  mshitakiwa alikana kosa na  kurudishwa  rumande  kwa  kushindwa  kukidhi  masharti  ya  dhamana na kesi itatajwa  tena Julai 6 mwaka huu.

WANANCHI WENYE HASIRA WAUWA MAJAMBAZI WATATU JIJINI ARUSHA

NA GLADNESS MUSHI -ARUSHA
 
 
WANANCHI wenye hasira katika eneo la Ngusero Ndani ya manispaa ya Arusha wamewaua majambazi matatu kwa silaha za jadi mara baada ya majambazi hayo kubainika kuwa wanapanga mbinu mbalimbali za kuvunja nyumba
Akiongea na waandishi wa habari mapema leo kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Bw Thobias Andengenye alisema kuwa tukio hilo lilitokea alfajiri ya saa kumi za asubui ambapo majambazi hayo yalifika katika eneo hilo huku yakiwa ndani ya gari
Kamanda Andengenye alisema kuwa mara baaada ya majambazi hayo kufika katika eneo hilo la tukio wakiwa na gari aina ya Corola lenye namba T830 AHU walianza kuzunguka zunguka katika eneo hilo ili kupanga nyumba ambayo wanaingia hali ambayo iliwashitua wananchi
Alifafanua kuwa mara baada ya wananchi kutilia shaka gari hilo ambalo lilikuwa na majambazi hao waliamua kuwaweka chini ya ulinzi na kukagua gari hilo ambapo walikutana na Silaha za jadi  pamoja na silaha nyingine ambazo ni za kuvunjia  nyumba hali ambayo ilisababisha waweze kupigwa sana na wananchi hao
“inavyosemekana ni kwamba hawa majambazi walikuwa wameshazunguka san a na gari lao kwa muda mrefu sana na sasa mara baada ya kuhisiwa wananachi waliamua kujichukulia sheria mkononi na kisha kuanza kuwapiga sana hali ambayo ilisababisha Mauti yao hapo hapo”alisema kamanda Andengenye.
Aliongeza kuwa mara baada ya Jeshi la Polisi kufika katika eneo hilo waliweza kugundua kuwa kati ya majambazi hayo matatu mawili yalikuwa yanatafutwa na jeshi hilo bila mafanikio kwa kuwa walikuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya unyanganyi wa kutumia silaha ndani ya maeneo mbalimbali ya Mji wa Arusha

Mkazi wa Arusha ashinda piki piki bahati nasibu ya Simba

Mwandishi wetu
SHABIKI wa timu ya soka ya Simba mkoani Arusha, Abubakar Hamis ameibuka kidedea katika droo ya bahati nasibu katika kampeni ya changia simba inayoendeshwa kwa ushirikiano baina ya Kampuni ya Push Mobile Media na klabu ya Simba.
Katika bahati nasibu hiyo Hamis ambaye ni dereva taxi amejinyakulia zawadi ya pikipiki yenye thamani ya zaidi ya shilingi milion tatu.
Kwa mujibu wa Meneja Kampeni wa Simba sms, Talib Rashid shabiki huyo ni miongoni mwa mashabiki zaidi ya 40 wa klabu hiyo kongwe hapa nchini waliojishindia zawadi mbalimbali ikiwamo pesa taslimu.
"Droo kubwa itafanyika Julai na mshindi atajinyakulia bajaji," alisema Rashid na kuongeza mashabiki wanatakiwa kuandika neno Simba na kutuma kwenda 15678 kuingia katika bahati nasibu hii.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema ushindi wa shabiki huyo ni uthibitisho tosha kwamba mashabiki wao wanashinda katika bahati nasibu hiyo.
"Naomba wanachama na mashabiki wetu wajitokeze kushiriki katika bahati nasibu hii kwani ni moja ya kuichangia klabu ya Simba iweze kujiendesha na kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya Tanzania," alisema Kamwaga.
Mshindi atazawadiwa zawadi yake ndani ya wiki mbili kuanzia sasa na kampuni ya Push Mobile Media itagharimia gharama za usafiri na kulala wakati wa kuja hapa jijini.
Alisema kuwa kwa sasa wamebakiza piki piki moja na bajaj ambazo drow yao itachezeshwa siku moja.

WAHINDU WA DHEHEBU LA SWAMINARAYAN WAFANIKIWA KUWATIBU WATOTO ELFU 17 KILA MWAKA NA KUWAPA MSAADA WANAFUNZI 4000 KILA MWAKA


BAADHI YA WANANCHI WA MJI WA ARUSHA WAKIWA KWENYE MSIKITI WA KITALII ULIOJENGWA NA WAHINDU
 
NA GLADNESS MUSHI -ARUSHA
Zaidi ya watoto elfu kumi na saba pamoja na wanafunzi 4000 ambao wanatokea katika mazingira magumu kila mwaka wanafanikiwa kupewa misaada mbalimbali ya kujikimu na Masomo huku watoto waliowagonjwa nao wanapewa msaada wa matibabu bure mpaka waweze kupona
Akiongea na waandishi wa habari mapema leo mwenyekiti wa Dhehebu la Swaminarayan ambao waumini wake wengi wanaasili ya kihundu,Bw Subash Patel alisema kuwa lengo ni kuwasaidia na kuwakomboa watoto wa kitanzania
Bw Subash alifafanuwa kuwa hali hiyo imekuja mara baada ya kuona kuwa watoto hao wana umuhimu mkubwa sana kwa jamii na pindi wanapokosa huduma za kielimu au matibabu imara basi huwa wanapoteza haki zao za msingi

TANZANIA YADHAMIRIA KUWEKA MAZINGIRA YA UPATIKANAJI WA MSAADA WA KISHERIA.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Dk. Alberic Kacou akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya  Mpango wa Msaada wa Kisheria Barani Afrika iliyoandaliwa na UNDP.
Dk. Kacou amesema warsha hii ya Msaada wa Kisheria ni hatua nyingine katika kuelekea kuondoa vikwazo katika uwezeshaji wa Kisheria na kupatikana kwa haki kitu ambacho kimeathiri kwa kiwango kikubwa bara hili katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na maisha ya watu, mali, Uraia, huduma za kijamii na kukosekana kwa fursa za maendeleo. Kulia ni Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Angela Kairuki
Dk. Kacou amesema warsha hii ya Msaada wa Kisheria ni hatua nyingine katika kuelekea kuondoa vikwazo katika uwezeshaji wa Kisheria na kupatikana kwa haki kitu ambacho kimeathiri kwa kiwango kikubwa bara hili katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na maisha ya watu, mali, Uraia, huduma za kijamii na kukosekana kwa fursa za maendeleo. Kulia ni Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Angela Kairuki na kushoto ni mmoja wa maafisa wa makao makuu ya UNDP New York Shelley Inglis.

Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Angela Kairuki akisoma hotuba wakati akifungua rasmi warsha ya  Mpango wa Msaada wa Kisheria Barani Afrika iliyoandaliwa na UNDP  na kuhudhuriwa na wadau wa masuala ya sheria kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wakiwemo wenyeji Tanzania.
Katia ufunguzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Mh. Kairuki amesema Serikali ya Tanzania imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha huduma za misaada ya Kisheria haswa kwa watu ambao ni vigumu kuupata msaada huo, ambao wengi wao wanaishi katika maeneo ya vijijini.
Kauli mbiu ya Warsha hiyo ni " Taking Forward Legal Aid Programming in Africa: Experiences and Lessons in Policy and Programming".
Baadhi ya wadau wa masuala ya sheria kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wakiwemo wenyeji Tanzania wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Mh. Angela Kairuki.

Miss Kigamboni City 2012 waanza kujinoa

Na Mwandishi Wetu

MAZOEZI kwa ajili ya kushiriki shindano la  kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012' yameshaanza mapema wiki hii imefahamika.
Shindano hilo limepangwa kufanyika ifikapo Juni 15 kwenye ukumbi wa Navy Beach ulioko huko Kigamboni hapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo jijini, Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya kinyang'anyiro hicho yanaendelea na warembo tayari wameshaanza mazoezi kwenye ukumbi wa Break Point ulioko Posta jirani na Club Billicanas.
Alisema kuwa bado milango iko wazi kwa warembo wenye sifa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini wanakaribishwa kushiriki kuwania taji hilo.
Aliongeza kuwa kampuni yake imejipanga kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa bora na kuwapata washiriki watakaokwenda kutwaa taji la Kanda ya Temeke na hatimaye taji la taifa la Redd's Miss Tanzania baadaye mwaka huu.
"Kila kitu ni maandalizi, tumejiandaa katika kufanya mchakato wa kupata warembo wenye sifa ili waweze kwenda kuiwakilisha vyema Kigamboni katika mashindano ya Kanda," alisema Somoe.
Aliwataja warembo ambao wameshaanza mazoezi kuwa ni pamoja na Caroline Peter, Theopisther Wenso, Sophia Martime, Amina Aboubakar, Aisha Rajab, Rosemary Peter, Mariam Mbulilo, Julieth Phili na Doreen Kweka.
Warembo hao wanafanya mazoezi chini ya Hawa Ismail ambaye alikuwa mshindi ya shindano la Kanda ya Temeke mwaka 2003.
"Bado tunakaribisha wadau wa sanaa ya urembo kutudhamini shindano hili, tunaamini uwepo wao ndio utafanikisha ubora na hadhi ya shindano letu mwaka huu kama tulivyodhamiria," aliongeza.
Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kudhamini shindano hilo ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF.
Taji la taifa la shindano hilo linashikiliwa na Salha Israel ambaye alitokea katika Kanda ya Ilala.

Makao Makuu ya Benki ya Azania kuhamia Mawasiliano Towers

 Na Mwandishi Wetu 
 
UONGOZI  wa benki ya Azania umeridhia uhamisho wa makao makuu ya benki hiyo kutoka Masdo House, mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam kwenda jengo la Mawasiliano Towers iliyopo mkabala na barabara ya Sam Nujoma kuanzia Jumatatu wiki ijayo kwa lengo la kuwatumikia wateja wa benki hiyo katika mazingira yenye nafasi ya kutosha. 
 
Hata hivyo, tawi la Masdo litaendelea kuwahudumia wateja waliopo katikati ya Jiji huko makao makuu mapya ya benki hiyo yaliyopo Mawasiliano Towers yakitoa huduma za kibenki kwa maeneo yaliyopo karibu na Ubungo, Mwenge ,Sinza na mengineyo. 
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa benki hiyo kwa vyombo vya habari jana, benki ya Azania itaendelea na mpango wake wa kujiimarisha zaidi kwa kuendelea kufungua matawi zaidi nchini ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kifedha karibu na watu na pia kuhakikisha usalama kwa pesa zao. 
 
Kupitia taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Charles Singili alisema benki yake ipo mbioni kufungua tawi jingine jipya katika Wilaya ya Geita na maeneo mengine yakiwemo Lamadi, Katoro na Kagongwa ifikapo mwisho wa mwezi ujao, hatua ambayo itasaidia kuimarisha uwepo wa benki hiyo katika kanda ya ziwa. 
 
 "Tunatarajia kufungua matawi mengine zaidi nchi nzima ifikapo mwisho wa mwaka huu ambayo yatasaidia benki yetu kuwa kitovu cha huduma za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini.
“Tangu benki ifunguliwe mwaka 1995, benki imekuwa haraka hali ambayo imesababisha mali za kampuni kufikia shilingi bilioni 190 mwishoni mwa mwaka 2011,” alisema Singili.
Singili aliongeza kuwa benki yake imelenga zaidi katika kutoa huduma za kibenki za kipekee kwa bei nafuu ukiilinganisha na mabenki mengine.
 “Nawahakikishia kwamba tutaendelea kutoa huduma za kipekee zinazokidhi mahitaji ya kila mteja wetu kwa upekee wake. Katika miezi sita iliyopita benki imejikita katika mpango madhubuti wa kujitanua kwa kufungua matawi matatu katika maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam, Arusha mjini katika barabara ya Wapare na mtaa wa sokoni jijini Moshi,” alisema.
 "Ninawaomba wateja wa benki ya Azania wa sasa na umma kwa ujumla kuendelea kupata huduma mbalimbali za kibenki na huduma zinazotolewa na benki hii ya Kitanzania yenye mafanikio," alisema.
Benki ya Azania iliaanzishwa mwaka 1995 kama  Adili Bancorp Limited baada ya Serikali kuruhusu mfumo wa uchumi wa soko huria  na kwa sasa benki hiyo ina wanahisa wakuu wakiwa pamoja na mashirika ya serikali yakiwemo, National Social Security Fund (NSSF) 34.8%, Parastatal Pensions Fund (PPF) 30.1%, Public Service Pensions Fund (PSPF) 17.2%, Local Authorities Pensions Fund (LAPF) 14.2%, na mengine.

JANUARI MAKAMBA AITAKA TCRA KUTATUA KERO ZA MAWASILIANO YA MITANDAO HARAKA

Naibu waziri wa Nishati na Madini January Makamba akiongea na waandishi wa habari leo hii katika makao makuu ya mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakati wa ziara yake katika makao makuu hayo, ambapo aliipa  TCRA wiki mbili kufuatilia na kujadili na kutoa taarifa juu ya kero za mawasiliano kwenye mitandao ya simu ikiwemo kukatika kwa network, pamoja na huduma za kuhifadhia pesa katika simu.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria katika ziara hiyo ya January Makamba.

Tigo waanzisha promosheni ya Xtreme Pack

Meneja wa Huduma za malipo ya kabla Tigo Bw, Suleiman Bushagama akizungumza na waandishi wa habari  leo hii makao makuu ya Tigo jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa promosheni mpya ya iitwayo Xtreme Pack ambapo mteja wa tigo anaweza kutuma meseji mbili za kulipia na kupata meseji tano za bure kwenda mitandao yote nchini.  
Kwakupiga *148*01# au kutumaneno XTREME kwenda namba 15509, wateja wa huduma yakulipia kabla watafurahia huduma za thamani ambazo ni pamoja na dakika 15 za muda wa maongezi zitakazowawezesha kupiga simu Tigo kwa Tigo, sms 100, 50 MB kwa ajili ya kuperuzi facebook, kutumia mtandao, E-mail pamoja na Twitter,vyote hivyo kwagharama ya Tsh 450 nakuokoa sh 4,600! Pia tigo itatuma ujumbe mfupi wa maneno bure kwa wateja wao, kuwataarifu juu ya ukomo wa matumizi ya vifurushi vyao na kuwaruhusu kujiunga tena kama watahitaji.
 Promosheni hiyo inaanza kutumika rasmi  kesho kushoto ni Titus Kafuma meneja wa Tigo internet na kulia ni  Alice Maro Msemaji wa Tigo, Naye afisa mahusiano wa Tigo Bi Alice Maro alisema kuwa wanatafuta njia thabiti ya kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata huduma zinazoendana na thamani ya pesa zao.
Mmoja wa waandishi wa habari Omary Katanga kutoka Redio one akiuliza swali kwenye mkutano huo pamoja na waandishi wa habari wengine wanaoonekana nyuma yake.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria kwenye uzinduzi huo wa Xtreme Pack ya Tigo.

Kamati ya PAC kutembelea waathirika wa Mabomu Mbagala Kuu

Katibu Mkuu  Ofis i ya Waziri Mkuu ,Peniel  Lyimo (katikati) akifafanua  jambo  wakati akitoa taarifa ya malipo ya waathirika ya mabomu  ya Mbagala  Mei 22,2012  katika Ofisi ndogo ya Bunge jijini  Dar- es -Salaam  alipowasilisha kwa Kamati ya  Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Mwenyekiti wake John Cheyo hayupo pichani, (kulia)  ni Mkurugenzi wa Idara ya Kitengo cha Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu  Meja Jenerali  Sylvester  Rioba, (kushoto ) Kaimu Katibu Tawala Mkoa DSM  Michael  Ole- Mungaya. Tukio la kulipuka kwa mabomu lilitokea mwaka 2009 huko Mbagala Kuu  Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha maafa kwa baadhi ya wakazi.(Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO).
Wajumbe wa kamati ya PAC wakiwa kwenye mkutano wa utoaji taarifa ya maafa ya Mabomu Mbagala chini ya Mwenyekiti  John Cheyo
Wakiangalia orodha ya malipo ya waathirika wa mabomu ya Mbagala
Muathirika Mzee Steven Gimongi (shoto) akitoa maelezo alivyoathirika wakati wa mabomu mbele ya Mk wa Kamati ya ( PAC )John Cheyo
Mwenyekiti wa( PAC) John Cheyo (koti) ,MP wa Kigamboni Dk. Faustin Ndugulile (kaunda) pamoja na baadhi ya wajumbe wa PAC na watenda
Mbunge wa Kigamboni Dr. Faustin Ndugulile (kaunda suti) akiwasikiliza baadhi ya waathirika wa mabomu huko Mbagala Kuu.

Rais Kikwete aongoza mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya mjini Dodoma

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri mkuu Mizengo Pinda na Wziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia wakiongoza Mafunzo ya Wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakuu wa wilaya yanayofanyika katika ukumbi wa St.Gaspar mkoani Dodoma.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati mafunzo ya wakuu wa mikoa,makatibu tawala na wakuu wa wilaya inayoendelea katika ukumbi wa St.Gaspar mkoani Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa na wilaya wanaoshiriki katika mafunzo katika ukumbi wa St.Gaspar mkoani Dodoma(picha na Freddy Maro)

Mkutano kundi la G77 and China katika mkutano wa mazingira jijini Bonn

Bi Fauzia Mwita, kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar, akishiriki katika majadililiano ya kuweka msimamo wa pamoja wa nchi zinazoendele katika mkutano wa kundi la G77 and China, katika mkutano wa mabadiliko ya Tabia nchi unaoendelea mjini Bonn.
Mkurugenzi wa mzingira zanzibar Bw Sheha Mjaja, akifuatilia mjadala wa kuweka msimamo wa pamoja wa nchi zinazoendelea katika mkutano wa kundi la G77 na China, kwenye Mkutano wa mabadiliko ya Tabia nchi unaendelea mjini Bonn
Bw. Ladsalus Kyaruzi, na Injinia Alphonce Bikulamchi Maafisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakishiriki katika majadiliano ya kuweka msimamo wa pamoja wa nchi zinazoendelea katika kundi la G77 na China.katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaoendelea mjini Bonn. (Picha na Evelyn Mkokoi)

Redds Miss Chan'gombe hiyooo yaja!!

Mashindano ya kuwania taji la Redds Miss Tanzania 2012 yanazidi kupamba moto kwa ngazi za vitongoji nchini kote huku vitongoji kadhaa vikiwa tayari vimesha fanya mashindano yake na vingine vikiendelea na maandalizi. 
Wakati wiki hii Mashindano hayo yakitraji kufanyika katika Vitongoji vya Kurasini Jijini Dar es Salaam tayari Wanyange wanaowania taji la Redds Miss Cha'gombe 2012  nao wapo katika mazoezi tayari kwa fainali zao zitakazo fanyika mapema mwezi ujao.
Pichani ni warembo wa Chan'gombe wakiwa katika picha ya pamoja iliyopigwa muda mfupi baada ya kumaliza mazoezi yao Mei 22,2012  katika ukumbi wa TCC Chan'gombe jijini Dar es Salaam.
Warembo hao 11 wanataraji kupanda jukwaani mapema mwezi ujao kuwania taji hilo na kuwania tiketi ya kushiriki Miss Temeke 2012.

Waziri Amos Makala akutana na wananchi kujadili mgogoro wa Ardhi Kinyenze

 Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makalla ( aliyesimama na kunyosha mkono juu) akisisitiza jambo juu ya namna ya kutafuta muakafa ili  kumalizwa kwa  mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kitongoji cha Kinyenzi dhidi ya Mwekezaji wa kizungu.
 Mzee Said Ahamad Kondo ( aliyesimama) akiuliza maswali  kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Mvomero , Amos Makalla ( hayupo pichani) alipokuwa katika  Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali kufuatilia mgogoro kati ya Wananchi hao na Mwekezaji wa Kizungu.
Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Jafari ( aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa  mgogoro wa shamba namba shamba 296  kati  ya wanachi wa Kitongoji cha Kinyenze na Mwekezaji wa Kizungu kwenye  mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makalla, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo , uliofanyika hivi karibini ( Mei 19) uliokuwa na lengo  la kufikia utatuzi wa mgogoro huo
Baadhi ya wazee na wananchi wa Kitogoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera,Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa Jimbo hilo, Amos Makalla ( hayupo pichani) wakati akipowatembelea hivi karibuni ( Mei 19) wananchi wa Kitongoji hicho kwa ajili ya kupanga mkakati wa kumalizwa mgogoro kati ya mwekezaji wa kizungu na wakazi hao, Mbunge huyo pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo.

No comments:

Post a Comment

Blog Archive